Home Mchanganyiko RMO KILIMANJARO AENDESHA OPERESHENI NA KUKAMATA TANI TATU ZA MADINI

RMO KILIMANJARO AENDESHA OPERESHENI NA KUKAMATA TANI TATU ZA MADINI

0
Ofisa madini mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Kyando akiandika taarifa za kazi ofisini kwake.
Ofisa madini mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Kyando akikagua madini ya yaliyokamatwa Kata ya Hedaru Wilayani Same yakisafirishwa kwenda jijini Dar es salaam bila kibali.
……………………………………..
TANI tatu za madini mchanganyiko yenye thamani ya sh15 milioni yamekamatwa Mkoani Kilimanjaro, mengine yakisafirishwa kwenda kuuzwa jijini Dar es salaam bila kuwa na kibali.
Ofisa madini mkazi wa mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Kyando alisema watu saba walikamatwa kwenye maeneo tofauti wakiwa na madini hayo. 
Kyando alisema watu watatu walikamatwa na madini aina ya Feldspar Carrot kwenye eneo la Hedaru wilayani Same wakitoa wilayani Simanjiro mkoani Manyara wakiyasafirisha jijini Dar es salaam. 
Alisema watu wawili walikamatwa wilayani Same wakiwa na madini ya vito aina ya Red garnet na Almandite bila kuwa na kibali cha aina yoyote kinachowapa haki ya kuwa na madini hayo. 
Alisema mjini Moshi waliyakamata madini tofauti ikiwemo vito mchanganyiko na madini ya viwanda na watu wawili ambao hawakuwa na kibali cha kuwa na madini hayo. 
“Tulishirikiana na askari polisi kwenye matukio hayo hapa Moshi na kule wilayani Same akiwemo OCCID na askari polisi wa kituo kidogo cha Hedaru katika kuwakamata watuhumiwa hao,” alisema Kyando. 
Mmoja kati ya wachimbaji madini wa mkoa huo, Godfrey Kiangi alipongeza ofisi ya madini ya mkoa wa Kilimanjaro kwa kazi kubwa wanayofanya na ushirikiano wanaotoa kwa wadau.
Kiangi alisema utendaji kazi wa ofisi ya madini Kilimanjaro ni mzuri kwani wanatoa huduma bora ikiwemo maelezo yaliyojitosheleza na utunzaji wa mazingira mzuri. 
“Hakuna urasimu kwenye ofisi zao na pia unaweza kupiga simu saa 24 ukapatiwa huduma kwani wanafanya kazi kwa vitendo bila ubaguzi wa kufahamiana hivyo wanastahili hongera kwa kazi nzuri wanayofanya,” alisema. 
Hata hivyo, aliwaasa wafanyakazi wa serikali wa ofisi nyingine kufanya kazi zao kwa kuiga mambo mazuri yanayofanywa na ofisi ya madini mkoani Kilimanjaro ambapo ukimaliziwa tatizo una hamu ya kurudi kwa namna huduma inavyotolewa.