Home Mchanganyiko WAWEKEZAJI WATAKIWA KUFUATA SHERIA,KANUNI NA UTARATIBU KUEPUKA UKINZANI NA SERIKALI

WAWEKEZAJI WATAKIWA KUFUATA SHERIA,KANUNI NA UTARATIBU KUEPUKA UKINZANI NA SERIKALI

0

*****************************

Na JUMA ISSIHAKA

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi Stella Manyanya, amewataka wawekezaji nchini kufuatilia sheria, kanuni na taratibu za uwekezaji  ili kuepuka ukiukwaji wa sheria na kusababisha ukinzani na taasisi za udhibiti za serikali. 

Hayo aliyasema wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya viwanda na Biashara mkoani Pwani ikiwa ni mara ya pili mfululizo kwa maonyesho hayo kufanyika mkoani humo. 

Alisema kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto za migogoro baina ya taasisi za udhibiti na wamiliki wa viwanda ambazo zinatokana na uelewa mdogo wa kanuni za uendeshwaji wa viwanda nchini.

“Wenye Viwanda wajibikeni kuhakikisha mnatambua taratibu za kisheria za uendeshaji na uanzishaji wa viwanda ili kupunguza migongano na taasisi za udhibiti, tunatambua kuwa wakati mwingine taasisi hizi nazo zinakuwa na matatizo hivyo tunafanya kila namna kukabili,” alisema.

Alizitaka taasisi za udhibiti kutowatoza faini wamiliki wa viwanda pasi na kuwapa maelezo ya kutosha kuhusu makosa yanayopelekea kutozwa faini hizo.

Mhandisi Manyanya, aliongeza kuwa maonyesho hayo yakatumike kama chachu ya kuvutia wawekezaji wengine kutokana na kukua kwa soko la bidhaa za viwanda nchini. 

BRELA

Akizungumza katika maonyesho hayo Msajili Mwandamizi wa Viwanda, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Yusuph Nakapala, alisema ushiriki wao katika maonyesho hayo ni kuhamasisha jamii kusajili kampuni na bidhaa zao. 

Alisema kwa sasa BRELA imewawezesha mfumo wa kusajili kampuni na biashara zao kwa njia ya mtandao kwa shabaha ya kuwapunguzia gharama na usumbufu wamiliki. 

“Sisi tupo hapa kutoa elimu kwa jamii juu ya kusajili kampuni zao na kama inavyojulikana kwamba kwa sasa tunafanikisha hilo kwa njia ya mtandao hivyo tunatarajia wenye viwanda wengi watatembelea banda la BRELA,” alisema. 

Aliongeza kwa kuzitaka kampuni zilizopewa siku 90 kukamilisha usajili kwa njia ya mtandao kufanya hivyo ndani ya muda huo na kwamba maonyesho hayo ndiyo fursa kubwa ya kupata elimu ya usajili kwa mfumo huo.

BRELA ilianza mfumo wa usajili kwa njia ya mtandano tangu Januari mosi mwaka jana na sasa ipo katika majaribio ya mfumo wa usajili wa leseni ya biashara daraja A.