*******************
Na Ahmed Mahmoud Arusha
Mkuu wa wilaya ya Arusha ,Gabriel Daqarro awataka walimu wa shule zote jijini hapa kutosita kuwaadhibu kwa viboko wanafunzi wenye nidhamu mbaya ili kurejesha nidhamu Mashuleni jambo litakalosaidia kuongeza ufaulu.
Gaqarro ametoa rai hiyo wakati akiongea na walimu wa shule mbalimbali za jiji la Arusha katika maadhimisho ya siku ya walimu duniani yanayofanyika Oktoba 5, kila mwaka ,yaliyoenda sanjari na kutoa zawadi za fedha tasilimu na vyeti kwa shule na walimu waliofanya vizuri.
Amesema suala la utii na nidhamu Mashukeni halina mjadala , hivyo walimu wanao wajibu wa kutumia viboko pale kunapolazimika bila kumwonea mwanafunzi na wasikubali wanafunzi kuwazoee.
“Ninacho waomba walimu ,mrejeshe nidhamu kwa wanafunzi na msikubali kuzoeana sana na mwanafunzi ,hiyo itasaidia ila msimwonee mwanafunzi na kutumia nguvu kupita kiasi hapo utakuwa umetenda jinai” Amesema Daqarro.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo aliagiza kutohamishwa ovyo kwa walimu bila kupewa fedha za uhamisho huku akiwataka walimu wanaoidai serikali kuwa wavumilivu wakati madai yao ya msingi yanashughulikiwa .
Awali walimu hao kupitia risala yao iliyosomwa na katibu Mkuu wa Chama cha walimu mkoa wa Arusha,CWT,Abraham Kamwela wameeleza changamoto mbalimbali zinazowakabilib ikiwemo mazingira ya kazi yao.
Pia wamedai kucheleweshewa kubadilishiwa mishahara yao kwani tangu wamepewa barua za mabadiliko ya mishahara bado mabadiliko hayo hayajafanyika ikiwemo suala la kupandishwa madaraja.
Aidha wameiomba halmashauri ya jiji la Arusha kuwakopesha viwanja ili wajenge nyumba za kuishi kwani baadhi yao wanaishi kwenye mazingira magumu na kujikuta wakikosa morari wa kufundisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa jiji la Arusha ,Dkt Maulid Madeni pamoja na kuwapongeza walimu hao kwa jitihada zao na kuufanya mkoa wa Arusha kuwa kinara wa ufaulu kitaifa amewaomba walimu hao wazidi kujituma zaidi huku akiahidi mazingira mazuri zaidi ya kazi yao.
Hata hivyo dkt Madeni amewatupia lawama kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo kwa kutowatendea haki walimu hao kwa kufanya mkutano wao usiku huku wakinyeshewa mvua na kung’atwa na mbu jambo ambalo aliahidi kipindi kijacho halmashauri yake itatoa fedha ili wafanyie kwenye kumbi za kisasa.
Dkt Madeni amewataka walimu hao kumkumbuka mwasisi wa taifa hili Hayati Mwl.Julius Nyerere ambaye ndio baba wa taifa hili aliyewatoa wananchi wake kwenye ujinga kwa kuhimiza elimu.
Amewataka pia walimu kumkumbuka rais John Magufuli ambaye serikali yake imefuta ada kwa shule zake nchini jambo ambalo limeongeza morari kwa wazazi kupeleka watoto wao kusoma.
Katika hatua nyingine dkt Madeni amesisitiza walimu kujiandikisha ili kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.