Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza
na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo wakati wa kikao
kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa
watumishi hao wilayani humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akifafanua
masuala ya kiutumishi kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Namtumbo (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao
kilichofanyika wilayani humo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Baadhi ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (hayupo
pichani) wakati wa kikao kazi cha waziri huyo na watumishi hao chenye
lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao wilayani humo.
*********************************
Na James K. Mwanamyoto, Namtumbo
10 Oktoba, 2019
Serikali imepiga marufuku taasisi za umma nchini kutumia fedha za Serikali
kuilipa taasisi binafsi ili kupatiwa huduma ambazo pia zinazotolewa na Mamlaka
ya Serikali Mtandao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) ametoa agizo hilo kwa
watumishi wa umma na waajiri Serikalini, wakati wa kikao kazi chake na
watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kilichofanyika wilayani humo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, Serikali imebadili Wakala ya Serikali Mtandao
kuwa Mamlaka kwa sababu hivi sasa ina wataalamu wa kutosha wa TEHAMA
hivyo hakuna ulazima wa kuilipa kampuni binafsi ili kupata huduma ya TEHAMA.
“Kama Serikali ina chombo chenye uwezo na weledi wa kutosha wa kutoa
huduma za TEHAMA ikiwemo mifumo ya kielektroniki ya utoaji huduma, ni nini
kinachoshinikiza Taasisi za Umma kuendelea kuomba kupatiwa huduma hiyo na
kampuni za watu binafsi?,” Mhe. Mkuchika amehoji.
Mhe. Mkuchika yuko katika ziara ya kikazi mkoani Ruvuma kwa lengo la
kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kukagua
utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani humo.