Home Mchanganyiko MAUAJI YA MWANAFUNZI YAZIDI KUWATESA WATUHUMIWA AMBAO NI WANAFUNZI WENZAKE

MAUAJI YA MWANAFUNZI YAZIDI KUWATESA WATUHUMIWA AMBAO NI WANAFUNZI WENZAKE

0
Na Silvia Mchuruza,Kagera;
WANAFUNZI wa shule ya Sekondari ya Katoro Islamic ya mkoani Kagera wanaotuhumiwa katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi mwenzao, Mudy Muswadiku wameshauriwa wawasiliane na Ofisi ya Elimu Mkoa wa Kagera na Mkuu wa Gereza ili waweze kupewa utaratibu utakaowawezesha kufanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.
Ushauri huo umetolewa leo katika kesiĀ  namba 18/2019 inayosikilizwa na Hakimu Frola Kaijage ilipotajwa kwa mara ya tatu katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba mkoaniĀ  na kuhairishwa tena hadi itakapotajwa tena Oktoba 15 mwaka huu.
Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Kagera, Haruna Shomari amesema kesi hiyo imehairishwa kwa sababu upelelezi bado haujakamilika na kuwa kuna maombi yametolewa kuwa wanafunzi hao walioko gerezani wafanye mtihani.
“Hilo ni jambo linalohusu kati ya Ofisi ya Elimu ya Mkoa na Mkuu wa Gereza, kwa sababu wako watu wanaoruhusiwa kufanya mtihani wakiwa gerezani, na wapo watu wamepata degree kwa kupata mafunzo wakiwa gerezani.
Kwa hiyo ni jambo ambalo linawezekana lakini utaratibu unaweza kufanywa kati ya Mkuu wa Gereza na Ofisi ya Elimu Mkoa,” alifafanua Wakili Shomari.
Wanafunzi hao tayari walisharuhusiwa kuendelea kujisomea wakiwa gerezani ili kujiandaa na mtihani wa kidato cha nne unaotarajiwa kuanza Novemba 4, mwaka huu nchini.
Kesi hiyo ya mauaji ya mwanafunzi huyo aliyekuwa anasoma kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic ya mkoani Kagera, inawakabili wanafunzi Sharifu Amri (19), Fahadi Abdulazizi Kamaga (20), Husama Ramadhan (17), Sharifu Huled (19), Abdalah Juma (19) na Hussein Mussa (20), Majaliwa Abud (35) mwalimu na Badru Issa Tibagililwa (27) mlinzi.
Mauji hayo yalitokea Aprili 14 mwaka katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic iliyoko katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera.
Watuhumiwa wamerudishwa rumande hadi siku kesi itakapotajwa tena kusubiri utaratibu upelelezi ukiwa umekamilika